Mwenyekiti

Imetupasa kulitangaza neno la Mungu kwa kila mtu; maneno yetu, matendo yetu – yaweza kuwa ujumbe wa wokovu kwa mtu fulani. Kufuata nyayo za Bwana wetu Yesu Kristo; kusaidia wengine kimwili, kiakili, kiroho – ingekuwa kipaumbele chetu kwa wakati huu. Ni kweli tumehubiri, tumegawa vitabu, tumetoa zaka na sadaka, lakini bado sio wote ambao tumetoka na kulitangaza Neno la Mungu kwa wengi wasiomjua Mungu

Mch: Mark W. Malekana

Shetani ametudanganya tujione kuwa tumeifanya kazi ya Mungu sana na sasa inatupasa kupumzika. Wakati umefika wa kila mmoja kuamka na kuingia shambani mwa Bwana kufanya kazi. Katika kitabu cha Tumaini la vizazi vyote uk. 142, ili kujenga au kukuza tabia kama ya Yesu ni lazima tufanye kazi kama alivyofanya; tunaweza kutembelea, kutoa msaada na pia kuhubiri. Tumekuwa na mikutano mingi ya injili, wengi wamempokea Mungu kwa njia ya ubatizo. Swali kubwa; Je, wewe ulishiriki?


Ninakutia moyo: Anza sasa! Hujachelewa. Mlete mmoja kwa Yesu. Unaweza kutoa mafundisho ya Biblia, unaweza kukaribisha watu kanisani, unaweza kuimba, unaweza kuhubiri, unaweza kutoa huduma nzuri ya tiba ya kimwili, na kupitia hapo mtu akamfahamu Kristo. Amini kuwa unaweza kuifanya kazi ya injili ya Mungu kwani Mungu ameahidi kuwa atakuwa pamoja nawe katika kazi.


Ni muhimu kutambua kuwa Mungu ana kazi kwa kila mmoja wetu. Jambo la muhimu ni kuamua sasa.  Unaweza kusema, “Mimi hapa nitume mimi!” Nawe utashangaa atakavyokuwezesha kuifanya kazi, hata pale ulipofikiri utashindwa atakuwezesha kuifanya. Ikiwa unafanya maamuzi sasa kushiriki kuifanya kazi ya Mungu Anza! Omba! Mwambie Mungu nahitaji kuwa Baraka kwa kuifanya kazi yako. Jitakase mbele zake, ndipo umuulize Mungu; Je, unataka nikufanyie nini?Mungu anasema, “Enendeni ulimwenguni kote mkayafanye mataifa kuwa wanafunzi wangu mkihubiri, mkifundisha na kubatiza.
 
ZINGATIA: Hakuna anayeachwa ni kila mmoja kushiriki kuhubiri injili. Kazi itakamilika pale tu kila mshiriki atakaposhiriki kuifanya kazi kikamilifu, kila mmoja amepewa talanta aweza kuitumia vyema kwa ajili ya utume. Mpendwa kama unataka kubarikiwa, shiriki katika kuifanya kazi ya Mungu nayo itakusaidia wewe mwenyewe kuwa vizuri katika maisha yako ya kiroho ; lakini pia itakuwezesha kuwa baraka kwa wengine katika kumfahamu na kumfuata Kristo.
“Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.” Zab 119:126