Katibu

Kanisa letu limekuwa likishuhudia mavuno mengi sana ya roho za watu kutokana na shughuli mbalimbali za uinjilisti. Lakini upande wa pili wa shilingi (mikakati ya malezi ya waumini hao wapya) umekuwa si mzuri sana.

Pr Magulilo Mwakalonge

Paulo alitahadharisha mapema juu ya kondoo wa Mungu kwa kusema, “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilonunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi. Tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi”- MATENDO 20:17, 28 – 31.

Neno ‘Jitunzeni’ linamaanisha kujilea, kujiangalia, na kuwa makini kwa roho zetu. Wito wa Paulo ni kuwa suala la malezi ya kiroho ni kwa kujilea sisi wenyewe pamoja na kundi ambalo Bwana ametupatia kuwa viongozi wao. Suala la malezi linahusiana sana na msingi wa kulifundisha neno la Kristo. Pia inaongeza kuwa malezi yanaambatana na kukesha. Kukesha maana yake nini? Ni kuomba kwa sala, dua, ibada, na maombi ya dhati kwa ajili ya wokovu wa roho zetu na roho za watu wengine. Hebu tufunge na kuomba kwa ajili ya kuombea maisha yetu ya kiroho na wengine pia.

Soma Ezekieli 11:17–21; 3:1 –9. Ulinzi unaozungumzwa hapa si maisha au uhai wa binadamu mwenzako bali ni ulinzi kwa ajili ya mashambulizi ya adui Shetani. Waumini wapo katikati ya pambano kuu kati ya wema na uovu. Hivyo ni kazi yetu kama binadamu kuchukuliana mizigo yetu sisi kwa sisi na kusaidiana katika safari ya kwenda Mbinguni. Hivyo kila muumini anahusika kikamilifu katika malezi ya waumini wapya na washiriki wa siku nyingi wanaokata tamaa katika safari. Mwongozo wa Wazee wa Kanisa, uk. 142: “Mwinjilisti (mhubiri), analinganishwa na mkunga (mzalishaji), Mchungaji analinganishwa na daktari wa watoto, na washiriki wa kanisa wanalinganishwa na familia.” [Mkunga na daktari wa watoto hawawezi kuachiwa kazi ya malezi. Malezi ni kazi ya familia].  “Wale ambao ni wapya katika imani ni lazima watunzwe kwa uangalifu mkuu na ni jukumu la waumini wazoefu kubuni njia na kujenga uwezo kuwasaidia, kuwahudumia, na kuwafundisha wale ambao wametoka kwenye makanisa mengine kwa ajili ya kuufuata ukweli, na hivyo kutengwa mbali na malezi ya kiroho waliyoyazoea”

Hivyo malezi ya washiriki ni jambo la kwanza kwa uongozi wa kanisa mara tu baada ya kwenda kuleta watu kwa Yesu Kristo. Hivyo wajibu wetu wote kama washiriki ndani ya kanisa ni kuwaleta watu kwa Kristo; na wajibu wa pili ni kuwa mlinzi wa ndugu zetu. Kuwalea na kuwatunza ni wajibu wa kwanza wa kujali roho yako na ya mwenzako. Usipojali walio nyumbani mwako, unakuwa mbaya kuliko mtu asiyeamini.

Kaini alidhani kwamba hatawajibika kwa kupotea kwake Abeli, lakini Mungu anatuonesha kwamba ulikuwa ni wajibu wake kumlinda ndugu yake. Kama tutafanya uzembe kuwalinda ndugu zetu kiimani hata Wakafa kifo cha kiroho, swali lile lile ambalo Kaini aliulizwa, sisi nasi – kila mmoja, ataulizwa, yuko wapi ndugu yako? Mwanzo 4:9